Subscribe Us

MBUNGE WA SUMBAWANGA

MBUNGE WA SUMBAWANGA
KARIBU KATIKA BLOG YETU YA WANA SUMBAWANGA KWA MATANGAZO NA HABARI PIGA SIM. 07577667558 AU 0713130507

HISTORIA YA SUMBAWANGA




kwenye neno Sumbu wanga, likiwa na
maana ya tupa uchawi , na lilianzishwa na
mtawala mmoja wa zamani wa eneo hilo
aliyeitwa Mwene Ngalu.
Sumbawanga ni makao makuu ya mkoani
Rukwa, uliopo Nyanda za Juu Kusini
Magharibi mwa Tanzania. Mkoa huu
unapakana na nchi za Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Zambia,
Burundi na mikoa ya Tabora na Mbeya na
una jumla ya watu milioni 1.5, kwa mujibu
wa sensa ya mwaka 2002. Ulianzishwa
rasmi mwaka 1972.
Mkoa huo una makabila mbalimbali ila kabila
kubwa na la asili ni Wafipa ambao ndiyo asili
ya jina Sumbawanga, mji ulioanzishwa
mwaka 1803, chini ya chifu wa kwanza wa
Ufipa aliyeitwa Kapufi ambaye alitawala
miaka ya 1885. Chifu Kapufi wa Kwanza
alianza milki yake ndani ya Ufipa yote na
makao yake makuu yalikuwa Kijiji cha
Kisumba nje kidogo ya mji wa Sumbawanga.
Mke wake aliitwa Mwene Wakulosi ambaye
walijaliwa kupata watoto watatu, wa
kwanza wa kiume na wawili waliofuata wa
kike ambao ni Mwene Kiatu wa pili aliitwa
‘Mwene Ngalu Chisichaafipa’ (jina la utawala)
na wa tatu aliitwa Mwene Mwati.
Baada ya kifo cha Chifu Kapufi wa Kwanza,
milki ilitawazwa kwa mwanae wa kwanza,
Mwene Kiatu ambaye alihamia kijiji cha
Lwiche ambako kwa mila na desturi za
kiutawala, ukitawazwa kuwa chifu ni lazima
uhame na kwenda kuanzisha kijiji chako
kama alivyofanya Mwene Kiatu.
Katika kipindi chake cha utawala wa eneo la
ufipa, chifu Mwene Kiatu hakujaliwa kupata
watoto na alipokufa, milki ilichukuliwa na
dada yake, Mwene Ngalu ambaye ndiye
mwanzilishi wa Sumbawanga.
Chifu Mwene Ngalu alikuwa mtu mwenye
upendo na hakupenda uchafu wa aina
yoyote ukiwamo uchawi, hivyo kabla ya
kuingia kijiji cha Sumbawanga
alichokianzisha, aliwataka wananchi
waliomfuata watupe uchafu wote kwenye
mto Lwiche pamoja na uchawi kisha
waingie wakiwa safi.
Kutokana na imani hiyo watu walitupa
uchawi wote na taka nyingine kisha
wakaingia kijiji cha Sumbawanga wakiwa
wasafi. Aliyekiuka amri hiyo na kuvuka mto
Lwiche kutaka kuingia kijiji kipya cha
Sumbawanga alikufa katika mto huo.
Hapo ndipo ikawa asili ya Sumbawanga na
kijiji kikawa na watu walio wasafi na
hakukuwa na matatizo na utawala wa
Mwene Ngalu. Alipendwa na kila ilipotokea
ishara ya matatizo ndani ya ufipa ilikuwa
rahisi kutatuliwa kwa kuwa Chifu Mwene
Ngalu aliomba na majibu yalipatikana
haraka, hasa kwa imani ya usafi waliokuwa
nao.
Hata hivyo Chifu Mwene Ngalu alijaliwa
kupata watoto saba ambao wote aliwazalia
katika nyumba yake ya utawala iliyojengwa
kwa kipindi cha miaka miwili katika mwaka
1918 hadi 1920 chini ya usimamizi wa
Mabruda wa dhehebu la Roma yaani
wakatoliki ambao walikuwa Wajerumani.
Nyumba hiyo hivi sasa imebomoka na
limebaki gofu ambalo kwa nje kuna sehemu
ya makaburi yanayotumika kuzika kizazi cha
utawala huo, na jambo la ajabu kwenye
gofu hilo wapo nyuki waliojenga kwenye
pango na wapo kwa muda mrefu tangu
kipindi cha uhai wa baadhi ya watawala wa
kizazi hicho.
Watoto wa Mwene Ngalu ni Maria wa Ngao,
Joseph Kapufi wa Ngao, Thadeo wa Ngao,
Teresia wa Ngao, Jacob wa Ngao, Victoria
wa Ngao na Antony wa Ngao, ambao baada
ya kifo cha mama yao, mtoto wa kwanza
Joseph wa Ngao alitawazwa kuwa Chifu wa
kizazi hicho na kupewa jina la Joseph wa
Ngao-Kapufi wa Pili.
Chifu huyo aliyejaliwa watoto wanne, ambao
ni Olanda Joseph, Adolf Joseph, Veneranda
Joseph na Yovita Joseph na alipofariki dunia
nduguye ambaye ni mdogo wake wa
mwisho, Antony wa Ngao alitawazwa
mwaka 1989, kuwa Chifu wa Ufipa na
kupewa jina la Kapufi wa Tatu.
Kapufi huyo wa tatu, Antony wa Ngao,
alitawala ufipa tangu mwaka 1989 hadi
Desemba 6 mwaka jana alipofariki dunia na
kuzikwa kwenye eneo la makaburi ya kizazi
cha utawala huo, karibu na jengo la Mwene
Ngalu ambalo hivi sasa limebaki gufo tu.
Katika kipindi cha utawala wake, Chifu
Kapufi wa Tatu, alijaliwa kupata watoto
watatu ambako mkewe wa kwanza alijaliwa
kupata mtoto mmoja wa kike aliyeitwa Ntalu
na mke mdogo alijaliwa kupata watoto
wawili wa kiume ambao ni Oscar na
Apolinary. Hata hivyo baada ya kifo cha
Kapufi wa Tatu, hivi sasa ukoo huo wa
kichifu uko kwenye mchakato wa kutafiti
mrithi wa kiti hicho.
Msemaji wa familia ya akina Kapufi Adolf
Joseph (61), ambaye ni mtoto wa Chifu
Joseph wa Ngao wa Pili, anasema jinsi ya
kumpata mrithi huyo ni kwa njia ya
kuwashirikisha wazee wa mji huo (wa
zamani) walio hai hivi sasa pamoja na wale
wa vijiji vya karibu kisha kuteua majina
kadhaa na kuyachambua kupata
anayestahili.
Anasema jina la mrithi likipatikana sherehe
za kumsimika kuwa Chifu wa kabila hilo
huanza kufanyiwa maandalizi, na kwa
kawaida hufanywa nje ya mji kwa
kutengeneza sehemu maalumu ya
kumpitishia ambayo huiita mzingo. Pia
huvuka mto Lwiche kwa imani kuwa ni
moja ya hatua za kudhihirisha kiwango cha
usafi wake kabla ya chifu mtarajiwa
kutawazwa.
Baada ya sehemu hiyo kukamilika
kutengenezwa chifu mtarajiwa hupitishwa
kwa nyuma kuingia kwenye mzingo huo
huku akipuliza filimbi tatu, ya kwanza
ikikataa kulia hupewa ya pili nayo ikigoma
hupewa ya tatu ambayo nayo ikigoma ni
dalili kuwa hafai kuwa chifu, hivyo
huenguliwa na kutafutwa mwingine.
Adolf anasema ikiwa filimbi moja au mbili
zikilia na moja kugoma watampa utawala
wa muda huku wakijiandaa kumtafuta chifu
mwingine, kwa imani kuwa filimbi zote
lazima zilie kwa sababu ni ishara ya sifa
njema za utawala za kiongozi anazopaswa
kuwa nazo ndipo apewe mamlaka.
Wakati mchakato huo ukiendelea, wa
kumpata mrithi wa kiti hicho, mavazi ya
Chifu Kapufi wa Tatu, Antony wa Ngao
amepewa Vicent Kafumu ambaye ni mjukuu
wa Chifu Mwene Ngalu kwa mzaliwa wake
wa kwanza aliyeitwa Maria wa Ngao.
Pamoja na hayo yote pia enzi za utawala wa
viongozi hao walitumia silaha mbalimbali
ambazo hadi leo baadhi yake zimehifadhiwa
ili mtawala ajaye akabidhiwe kwa ajili ya
kudumisha mila. Zana hizo ni upinde
(ulapwa), mishale (ncheto), fimbo (wasi),
mkuki (ilawa) na chombo cha kubebea
mishale (untontowaancheto). Silaha
nyingine ni shanga (inkasi) zinazovaliwa
mikononi na shingoni kwa chifu, kiti cha
miguu mitatu (kisumbi) na vazi la kujifunga
kiunoni na mabegani (seketa) ambayo
husukwa kwa pamba.
Anasema mabadiliko ya dunia na teknolijia
na mapinduzi ya kilimo kwa kiasi kikubwa
zilibadilisha mtazamo na fikra za wakazi wa
Sumbawanga ambako muingiliano wa watu
ulipoanza imani ya uchawi na ushirikina
zilipungua na watu wakaingia katika
shughuli za uzalishaji mali ingawa baadhi
yao wanaendelea na ushirikina kama zilivyo
sehemu nyingine nchini.
Mabadiliko hayo pia yalipunguza nguvu ya
kuabudu mizimu iliyokuwapo hapo awali
kwa kuwa misitu mingi ilifyekwa kwa ajili ya
shughuli za kilimo na ufugaji hivyo, imani ya
kuwapo mizimu iliondoka kwa asilimia
kubwa na watu wakabakia kuabudu katika
nyumba za ibada kufuatana na imani ya dini
zao, anasema Adolf.
Hata hivyo bado kuna sehemu au vijiji
vyenye kuendelea kuamini mizimu na
ushirikina kama vile kijiji cha Chipu kilicho
kilomita kama 30 kutoka Sumbawanga mjini
na vijiji vya Milanzi na Kalambo ambavyo
bado imani ya uchawi na vitendo vya
kishirikina vinaendelea kwa baadhi ya
wakazi wake.
Kwa kijiji cha Milanzi baadhi ya wakazi wake
hutumia mapango yaliyo kwenye mlima
uitwao Itwelele kwa kufanya matambiko na
mambo mengine ya kishirikina kwa imani
kuwa mizimu iliyopo huko huwasaidia
kutekeleza mahitaji yao na kumdhuru mtu
au watu waliotenda makosa na kuyakana.
Adolf anasema hilo siyo tatizo kubwa kwa
sababu hakuna anayemdhuru mgeni
anayeingia mkoani hapo kwa kufanya
shughuli zake kama vile biashara au kilimo.
Ila kwa wale ambao hawajafika
Sumbawanga hudhani kuwa huo ni uchawi
na ushirikina tu, dhana ambayo si ya kweli
kwa kuwa maendeleo yanayopatikana
katika karibu makabila yote nchini hivi sasa
yapo pia Sumbawanga

10 comments:

  1. Safi saaana kwa historia
    Naomba siku moja niwasilishe ombi langu kwako tuone tunafanyaje

    ReplyDelete
  2. Nimefarijika sana kusoma historia ya Wafipa na asili ya jina la Mji wa Sumbawanga, inafurahisha sana .
    Mimi pia niliwahi kusimuliwa habari za Mwene Ngalu alipotakiwa kuonesha mipaka ya utawala wake kama mwandishi alivyoeleza.
    Nilichobaini, Wafipa tulio wengi tuna tabia ya kujificha;hatutaki tujulikane kabila letu la wafipa.
    Sumbawanga kwa sasa imepiga hatua kubwa kimaendeleo kifikra na kitamaduni kwa sababu muingiliano wa watu toka sehemu mbalimbali za nchi kufuata fursa zilizopo Sumbawanga,licha ya changamoto zilizopo za umaskini, miundo mbinu, umeme, maji, huduma duni za afya,elimu,usafiri wa anga na Tekinolojia ya njia za mawasiliano.Hata hivi, Sumbawanga ni pazuri kwa kuishi gharama ziko chini tofauti na sehemu nyngine za nchi yetu.

    ReplyDelete
  3. Kabla ya Mwene Ngalu alitawala Mwene Kapere (Ntinda)wakati wa utawala wa wajerumani 1897-1905 alipotafautiana na utawala wa kijerumani alikimbia ndipo akatawazwa Mwene Ngalu na baada ya Mwene Ngalu alitawala tena Mwene Kapere 1937-1958 katika utawala wa Waingereza baada ya hapo ndiyo akatawazwa Mwene Kapufi II mtoto wa Mwene Ngalu na ndiyo alitawala mpaka kipindi cha Uhuru wa Tanganyika...NB nini kilifanya Mwene Kapere akosane na wajerumani na kukimbia na kisha kurudi wakati wa utawala wa Uingereza nitaweka wazi rasmi.

    ReplyDelete
  4. Mungu akubariki sana uliyetoa historia" HISTORI IS A GOOD TEACHER BUT HAS POOR STUDENTS"

    ReplyDelete
  5. Kumbe jina la sumbawanga ni jina zuri nilikuwa sijajua chimbuko lake wafipa hongereni kwa kudumisha mila na desturi zenu

    ReplyDelete
  6. Nimefurai Sana kupata hisitoria hii Mim ni mfipa Ila nimezaliwa kigoma na kukulia kigoma najifunza taratibu Mira na nesturi za kabila langu mtoastori hongera Sana,

    ReplyDelete
  7. Historia nzuri sana! Andika kitabu na pia ongeza habari za kina mwene kapere.

    ReplyDelete